Manchester United inaripotiwa kujiandaa kikamilifu kutumia fursa ya kupungua kwa bei ya kiungo wa West Ham United, Mateus Fernandes, ili kuinasa saini yake msimu huu wa joto, licha ya kukabiliwa na ushindani mkubwa kutoka kwa miamba ya Uhispania, Real Madrid.
Mashetani Wekundu tayari wamefikia makubaliano na klabu ya Atalanta kwa ajili ya kumsajili kiungo Ederson kwa ada ya pauni milioni 35. Hata hivyo, klabu hiyo bado ipo sokoni kusaka viungo wengine zaidi kufuatia kuondoka kwa Casemiro baada ya mkataba wake kumalizika, huku kiungo wa kimataifa wa Uruguay, Manuel Ugarte, naye akitarajiwa kufungashiwa virago huko Old Trafford.
Fernandes, ambaye ana umri wa miaka 21 pekee, alijiunga na West Ham msimu uliopita wa joto akitokea Southampton kwa ada ya pauni milioni 40. Amekuwa mmoja wa wachezaji wanaopewa kipaumbele kikubwa na United, na ripoti za hivi karibuni zinafichua kuwa wawakilishi wa mchezaji huyo wana imani kubwa ya kufikia makubaliano yatakayomwezesha kutua Old Trafford.
Ushindani kutoka Real Madrid na Jose Mourinho
Hali ya usajili wa Fernandes inazidi kuwa ya kuvutia kutokana na nia ya dhati kutoka kwa Jose Mourinho. Mourinho anahusishwa na kiti cha ukocha cha Real Madrid baada ya Rais Florentino Perez kushinda uchaguzi wa kuiongoza klabu hiyo dhidi ya mpinzani wake, Enrique Riquelme.
Inaarifiwa kuwa Mourinho ametoa ombi maalum kwa uongozi wa Real Madrid kufanya kila liwezekanalo ili kumsajili Fernandes msimu huu, hatua inayoongeza presha kwa Manchester United kukamilisha dili hilo mapema.
Kuporomoka kwa Bei ya Fernandes
Kufuatia kushuka daraja kwa West Ham kutoka Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), Fernandes ameweka wazi kuwa anataka kuondoka klabuni hapo. Hali hiyo imewalazimu West Ham kuweka bei ya pauni milioni 80 kwa kiungo huyo ili kuzuia klabu kubwa kumchukua kirahisi.
Hata hivyo, skauti wa zamani wa West Ham, Mick Brown, anasisitiza kuwa dau hilo lililowekwa na Wagonga Nyundo hao litashuka kadiri dirisha la usajili linavyozidi kusonga mbele, jambo ambalo litaipa United nafasi nzuri ya kushambulia.
"Itakuwa vigumu sana kwa West Ham kumbakisha Fernandes. Kimsingi, wangependa kubaki naye na angekuwa nguzo muhimu ya timu katika harakati za kupambana kurejea Ligi Kuu ya Uingereza."
Brown aliongeza kuwa hali huwa ngumu sana kwa klabu zinazoshuka daraja:
"Lakini mambo si rahisi hivyo; inakuwa mtihani mkubwa sana pale klabu inaposhuka daraja, na mara nyingi wanalazimika kuruhusu wachezaji kuondoka kwa sababu hawawezi kumudu gharama za kuwabakisha. Nimeambiwa wameweka bei kubwa kwa Fernandes, lakini kushikilia msimamo wa bei hiyo ndiyo itakuwa changamoto kubwa. Mchezaji hatataka kubaki kucheza Ligi ya Championship."
Fursa ya Dhahabu kwa Manchester United
Fernandes alikuwa mmoja wa wachezaji bora zaidi wa West Ham kwenye Ligi Kuu msimu uliopita na alionyesha kiwango cha hali ya juu, hali inayofanya klabu za hadhi ya juu kuanza kummezea mate.
Brown anaamini kuwa United itasubiri muda muafaka ili kupata mchezaji huyo kwa bei ya punguzo:
"Dirisha la usajili likiendelea na ikionekana wazi kuwa anataka kuondoka, thamani yake itashuka, na klabu kama Man United inaweza kutumia mwanya huo. United hakika ni miongoni mwa klabu zinazovutiwa naye, hivyo watakuwa wakifuatilia kwa karibu hali yake na wanaweza kutuma ofa rasmi ikiwa makubaliano yatakuwa ya kirafiki kifedha."
Kwa sasa, macho yote ya mashabiki wa soka nchini Tanzania na duniani kote yapo kwenye dirisha hili la usajili kuona kama Mashetani Wekundu watafanikiwa kuipiku Real Madrid katika mbio za kuwania saini ya kinda huyo mwenye kipaji kikubwa cha kusambaza mipira dimba la kati.