Kocha mkuu mpya wa Liverpool, Andoni Iraola, ameweka wazi kuwa anatarajia kufanya makubwa na beki wa kushoto wa timu hiyo, Milos Kerkez, huku akimtaja kama mchezaji wa kwanza anayetaka kumsaidia kuimarika zaidi uwanjani Anfield.
Iraola ameteuliwa rasmi kuinoa miamba hiyo ya soka ya Uingereza kufuatia kufukuzwa kazi kwa aliyekuwa bosi wa timu hiyo, Arne Slot. Mhispania huyo mwenye umri wa miaka 43 anawasili Anfield akiwa na wasifu mzuri, baada ya kuiongoza Bournemouth kufuzu michuano ya Europa League kwa msimu wa 2026/27.
Wakati wa kibarua chake huko Bournemouth, Iraola alifanikiwa kufanya kazi kwa karibu na Kerkez, ambaye baadaye alijiunga na Liverpool akitokea kwa 'The Cherries' msimu wa joto wa mwaka 2025 kwa ada ya pauni milioni 40.
Changamoto ya Milos Kerkez Ndani ya Anfield
Akiwa chini ya Iraola kule Bournemouth, Kerkez alijitengenezea jina na kuwa mmoja wa mabeki bora wa kushoto wenye kasi na uwezo mkubwa kwenye Ligi Kuu ya Uingereza. Hata hivyo, mambo hayakuwa rahisi kwake baada ya kutua Anfield.
Msimu wake wa kwanza ndani ya jezi ya Liverpool ulitajwa na wengi kuwa wa kusuasua na chini ya kiwango kilichotarajiwa. Beki huyo wa kimataifa wa Hungary mwenye umri wa miaka 22 alilazimika kupambana vikali kupata nafasi ya kuanza mbele ya mkongwe Andy Robertson. Licha ya changamoto hizo, Kerkez alifanikiwa kuanza kwenye michezo 27 ya Ligi Kuu na mechi saba za Ligi ya Mabingwa Ulaya chini ya ukufunzi wa Slot katika msimu wa 2025/26.
Sasa, kufuatia kuwasili kwa kocha wake wa zamani, milango ya matumaini imeanza kufunguka upya kwa kijana huyo. Iraola amemnyooshea kidole Kerkez kama mradi wake wa kwanza kabisa wa maboresho kikosini.
Iraola Afunguka Mipango Yake Anfield
Akizungumza na tovuti rasmi ya Liverpool, Iraola alulizwa kama kufuatilia soka la Ligi Kuu kwa karibu akiwa Bournemouth kutampa faida katika kuanza maisha yake mapya Anfield. Kocha huyo alijibu:
"Ndiyo, kwa hakika kabisa. Kwangu mimi, ni rahisi zaidi kuendelea kufanya kazi kwenye Ligi Kuu ya Uingereza kwa sababu tayari navifahamu vikosi vizuri sana."
"Tumeisoma sana Liverpool huko nyuma—tulichambua udhaifu wao unaoweza kujitokeza, na pia nguvu zao. Nafikiri tuna kikosi kizuri sana hapa."
"Najua bado kuna kazi kubwa ya kufanya, kama ilivyo kawaida kwa kila klabu katika kipindi hiki cha msimu. Lakini kwa sasa, kitu cha muhimu zaidi kwangu ni kuwapa thamani kubwa wachezaji tulionao sasa kwenye kikosi."
Iraola aliongeza kuwa anawatazama wachezaji wote waliopo sasa kama wachezaji wapya kabisa na ana shauku ya kuanza nao kazi, huku akimzungumzia Kerkez kwa upekee:
"Nitawaambia wachezaji kuwa wote ni kama usajili mpya kwangu. Tuna ubora mkubwa sana kwenye kikosi chetu, na nina shauku kubwa ya kuanza kufanya nao kazi. Katika kikosi hiki, nadhani ni Milos pekee niliyewahi kuwa naye hapo awali—ingawa nawafahamu wachache na nimeshaongea na baadhi yao kabla ya hapa. Lakini itakuwa jambo zuri sana kufanya kazi tena na Milos, kujaribu kumboresha na kumsaidia katika ukuaji wake. Kwa kweli, nina shauku kubwa ya kuanza hili."
Heshima Kubwa kwa Arne Slot na Ndoto za Ligi ya Mabingwa Ulaya
Pamoja na kuanza mikakati mipya, Iraola hakusita kumpigia saluti mtangulizi wake, Arne Slot, ambaye aliiongoza Liverpool kutwaa taji la Ligi Kuu ya Uingereza msimu wa 2024/25 kabla ya mambo kumharibikia msimu uliofuata.
"Ndiyo, nina heshima kubwa sana kwa Arne, heshima ya dhati kabisa. Amewahi kuwa bingwa wa Premier League na hili ni jambo kubwa sana, hasa kwa klabu kubwa kama Liverpool," alisema Iraola.
Mbali na hayo, kocha huyo alizungumzia fursa ya kuiongoza Liverpool kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya (UEFA Champions League), jambo ambalo hajawahi kulifanya kama kocha hapo awali.
"Kuhusu Ligi ya Mabingwa, nilipata nafasi ya kucheza michuano hii mara moja tu nikiwa mchezaji. Tulizoea kufuzu sana michuano ya Europa League (akiwa na Athletic Club), lakini Ligi ya Mabingwa nilicheza mara moja tu. Sasa nina shauku kubwa ya kucheza kwa mara ya kwanza nikiwa kocha. Kuna mahitaji makubwa na changamoto kubwa, lakini pia kuna fursa kubwa ya kukabiliana na timu bora zaidi barani Ulaya na kuona wapi tulipo."
Mashabiki wa Liverpool sasa wanasubiri kwa hamu kuona kama muunganiko huu mpya kati ya Iraola na beki wake wa zamani Kerkez utarudisha makali ya mlinzi huyo na kuisaidia timu hiyo kurejea kwenye kilele cha soka la Uingereza na Ulaya.