Harakati za Aston Villa Sokoni
Klabu ya Aston Villa ipo kwenye maandalizi makubwa ya kujipanga upya kwa ajili ya msimu ujao, huku ripoti zikisema kuwa wameanza kusaka wachezaji watatu wapya kuziba pengo la nyota wanaotarajiwa kuondoka. Kubwa zaidi linaloteka vichwa vya habari ni makubaliano ya maslahi binafsi kati ya golikipa wao tegemeo, Emiliano Martinez, na miamba ya soka ya Italia, Juventus.
Chini ya kocha wao mahiri Unai Emery, Villa walikuwa na msimu mzuri wa 2025/26 ambapo walifanikiwa kumaliza katika nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Uingereza (Premier League) na kutwaa ubingwa wa kihistoria wa michuano ya Europa League. Hata hivyo, mafanikio hayo sasa yameleta changamoto mpya ya kulinda nyota wao wasiondoke, huku wachezaji kama Morgan Rogers wakivutia klabu nyingi kubwa.
Zion Suzuki Kuvaa Viatu vya Emiliano 'Dibu' Martinez?
Kipa wa timu ya taifa ya Argentina, Emiliano Martinez, ambaye alitarajiwa kuondoka Villa Park msimu uliopita, mara nyingine tena anahusishwa na mlango wa kutokea. Safari hii, Juventus wameonekana kuwa makini zaidi kukamilisha dili lake.
Kufuatia uwezekano mkubwa wa Martinez kuondoka, Aston Villa hawataki kulala. Habari kutoka kwa mwandishi wa habari za michezo wa Italia, Nicolo Schira, zinaeleza kuwa klabu hiyo tayari imtuma maskauti wake kumtazama mlinda mlango wa timu ya taifa ya Japan na klabu ya Parma, Zion Suzuki.
Schira aliandika kupitia ukurasa wake wa X (zamani Twitter):
"Exclusive - Maskauti wa Aston Villa walikuwa Dallas kutazama mechi ya Kombe la Dunia kati ya Uholanzi na Japan ili kumfuatilia golikipa wa Parma, Zion Suzuki, ambaye anapewa nafasi kubwa ya kumrithi Emiliano Martinez. 'El Dibu' yuko tayari kuondoka msimu huu wa joto na amekubali maslahi binafsi na Juventus."
Alex Remiro Kwenye Orodha ya Villa
Mbali na Suzuki, Villa pia wanatupia jicho nchini Uhispania ambako mlinda mlango wa Real Sociedad, Alex Remiro, anatajwa kama mbadala mwingine madhubuti. Ripoti kutoka gazeti la Express and Star zinasema:
"Villa wamekuwa wakimfuatilia kwa karibu mlinda mlango wa Real Sociedad, Alex Remiro, huku kukiwa na mashaka juu ya mustakabali wa Emi Martinez. Remiro, ambaye ameichezea Uhispania mara mbili, ni miongoni mwa makipa kadhaa wanaofikiriwa iwapo Martinez ataondoka na klabu ikalazimika kuingia sokoni."
Mapinduzi ya Ushambuliaji: Serhou Guirassy Anukia Villa Park
Kwenye eneo la ushambuliaji, Aston Villa wanahusishwa kwa karibu na mshambuliaji hatari wa Borussia Dortmund, Serhou Guirassy. Licha ya uvumi uliokuwa ukisema kuwa amekubali kujiunga na Fenerbahce ya nchini Uturuki, kaka na wakala wa mchezaji huyo, Karamba Guirassy, amekanusha taarifa hizo vikali kupitia vyombo vya habari vya Ujerumani.
Karamba Guirassy aliiambia Sky Germany:
"Ili kuweka mambo sawa: hakuna makubaliano ya aina yoyote yaliyofikiwa. Serhou kwa sasa anafanya tathmini ya nafasi alizonazo kwa ajili ya msimu ujao. Madai yoyote ya makubaliano ya mdomo si ya kweli hata kidogo."
Mwandishi wa habari Patrick Berger ameongeza kuwa Aston Villa ni miongoni mwa timu zinazopigana vikumbo kumnasa mshambuliaji huyo, akisema:
"Mbali na Fenerbahce, klabu kadhaa zikiwemo Aston Villa, Tottenham Hotspur, AC Milan na Atletico Madrid zimemweka Guirassy kwenye orodha yao ya usajili. Lakini bado hakuna makubaliano yaliyofikiwa wala uamuzi uliotolewa. Kuondoka Dortmund msimu huu bado ni jambo linalowezekana sana."
Lloyd Kelly Kuimarisha Safu ya Ulinzi
Katika kuimarisha idara ya ulinzi, beki wa zamani wa Bournemouth na Newcastle United, Lloyd Kelly, ambaye kwa sasa anakipiga Juventus, yupo kwenye rada za Villa. Kwa mujibu wa mtandao wa michezo wa Italia, TuttoJuve, Villa inasemekana kuwa kwenye "mstari wa mbele" kujaribu kurejesha mlinzi huyo nchini Uingereza ili kuongeza uzoefu na nguvu kwenye safu yao ya ulinzi msimu ujao.
Mashabiki wa Aston Villa wanasubiri kwa hamu kuona jinsi kocha Unai Emery atakavyocheza karata zake sokoni ili kuhakikisha kikosi hicho kinaendelea kuwa tishio si tu nchini Uingereza bali pia kwenye anga za soka la Ulaya.