Mambo yamezidi kuwa magumu ndani ya klabu ya West Ham United. Baada ya klabu hiyo kukumbana na janga la kushuka daraja kutoka Ligi Kuu ya Uingereza (Premier League) hivi karibuni, sasa imekumbana na pigo jingine kubwa nje ya uwanja.
Mwenyekiti mwenza wa klabu hiyo, David Sullivan, ametangaza kujiuzulu nafasi yake mara moja kufuatia taarifa za kuwepo kwa tuhuma nzito dhidi ya maisha yake binafsi zinazotarajiwa kuchapishwa hivi karibuni kwenye vyombo vya habari. Sullivan amezitaja tuhuma hizo kuwa ni "za uongo, zisizo na ukweli wowote na za miongo kadhaa iliyopita."
Mfanyabiashara huyo mwenye umri wa miaka 77 pia ameachia ngazi kama mkurugenzi wa kampuni ya WH Holding Limited pamoja na klabu ya West Ham yenyewe, hatua inayokuja wakati klabu hiyo ikijiandaa na maisha mapya baada ya kushuka daraja katika siku ya mwisho ya msimu.
Katika taarifa yake ndefu kwa umma, Sullivan alieleza kuwa amepata taarifa za kuwepo kwa ripoti inayolenga kuanika tuhuma hizo za zamani kuhusu maisha yake binafsi, na ameamua kuchukua hatua madhubuti kulinda jina lake.
"Madai ya uongo yaliyoelekezwa dhidi yangu yamekuwa yakikuuzwa na kupewa sifa kubwa ya kishabiki na vyombo vya habari," alisema Sullivan.
"Baada ya maisha yangu yote niliyotumia kujenga biashara katika sekta ya burudani ya watu wazima ambapo nimekutana na maelfu ya wanawake, kwa masikitiko makubwa haiwezi kuepukika kwamba idadi ndogo ya madai ya tabia isiyofaa yatatolewa dhidi yangu. Ninakanusha kabisa madai haya."
Vita vya Kisheria Dhidi ya BBC
Kiongozi huyo wa zamani wa Hammers ameweka wazi kuwa hatakaa kimya na badala yake anajipanga kupambana mahakamani. Sullivan ametangaza kuwa anajiandaa kulifungulia mashtaka ya kashfa shirika la utangazaji la BBC, pamoja na chombo kingine chochote cha habari kitakachothubutu kurudia au kusambaza tuhuma hizo anzoziita za kusingizia.
Shirika la habari la Reuters limeripoti kuwa limejaribu kuwasiliana na BBC ili kupata upande wao wa mada lakini bado hawajatoa majibu rasmi.
West Ham Yajitenga na Tuhuma Hizo
Kwa upande wao, West Ham United wameweka wazi kuwa tuhuma hizo hazihusiani hata kidogo na klabu hiyo au uendeshaji wake wa kila siku. Klabu imetangaza kuwa shughuli zote za uongozi zitaendelea kama kawaida chini ya usimamizi wa Mtendaji Mkuu wa Muda.
"Mtendaji Mkuu wa Muda, Karim Virani, akiripoti kwa Bodi ya Wakurugenzi ya sasa, ataendelea kuwa na jukumu la kuongoza shughuli za kila siku za klabu," ilieleza taarifa rasmi ya West Ham.
"Klabu itatoa taarifa rasmi kuhusu muundo wa baadaye wa Bodi ya Wakurugenzi kwa wakati unaofaa."
Uamuzi Mgumu kwa Mapenzi ya Klabu
Sullivan alieleza kuwa uamuzi wake wa kujiuzulu ulikuwa wa "maumivu makubwa sana" lakini ulikuwa ni wa lazima ili kulinda maslahi ya West Ham, hasa katika kipindi hiki kigumu ambapo timu hiyo inajiandaa kucheza ligi ya daraja la kwanza (Championship) kwa mara ya kwanza tangu msimu wa 2011-12.
"Hakuna hata moja ya tuhuma hizi inayohusiana na zaidi ya miaka yangu 30 niliyotumia kwenye soka; West Ham United imekuwa moja ya mapenzi makubwa na heshima kubwa katika maisha yangu," aliongeza Sullivan.
"Ninaijali sana klabu hii, mashabiki wake, wachezaji wake, wafanyakazi wake na hatma yake. Katika kipindi hiki ambacho tayari kina changamoto nyingi na muhimu kwa klabu, ninakataa kabisa kuruhusu mambo yangu binafsi kuwa kero isiyo ya lazima au chanzo cha kukosekana kwa utulivu wa timu."
Mzee huyo mwenye ushawishi mkubwa amesisitiza kuwa sasa ataelekeza nguvu zake zote kupambana kisheria ili kusafisha jina lake.
"Ninajiuzulu ili kuelekeza nguvu zangu zote na umakini wangu katika kupambana na tuhuma hizi za uongo. Nimeshaajiri rasmi timu yangu ya wanasheria na tunajiandaa kuanzisha mashauri ya kisheria dhidi ya kila malalamiko ya uongo yaliyotolewa dhidi yangu. Nitatafuta haki kamili kisheria na hadharani katika kila nyanja."