Beki wa zamani wa Manchester United, Gary Neville, anaamini kuwa usajili wa mshambuliaji wa Chelsea, Cole Palmer, utakuwa kama "dhahabu safi" kwa Mashetani Wekundu, ingawa ana wasiwasi mkubwa kama matajiri hao wa London watakuwa tayari kukubali mpango huo wa mamilioni ya pauni.
Palmer alihusishwa sana na mpango wa kuondoka Stamford Bridge kuelekea mwishoni mwa msimu uliopita, huku kukiwa na taarifa kuwa hakuwa na furaha klabuni hapo na alikuwa akishinikiza kurejea jijini Manchester.
Nyota huyo mwenye umri wa miaka 24 alipitia kipindi kigumu cha kupoteza fomu na majeraha katika nusu ya kwanza ya msimu, lakini bado alifanikiwa kumaliza msimu akiwa amepachika mabao 10 ya Ligi Kuu ya Uingereza (Premier League). Hata hivyo, Chelsea ilikuwa na msimu mbaya ikishinda mchezo mmoja tu kati ya nane ya mwisho na kumaliza katika nafasi ya 10 kwenye msimamo wa ligi.
Kutokana na mdororo huo wa kiwango cha klabu yake, Palmer alilipia gharama kubwa baada ya kuachwa nje ya kikosi cha timu ya taifa ya Uingereza kilichoteuliwa na kocha Thomas Tuchel kwa ajili ya Kombe la Dunia linalotarajiwa kufanyika Amerika Kaskazini.
Usajili wa "Dhahabu Safi" Kama wa Enzi za Sir Alex
Pamoja na kushuka kwa thamani yake sokoni hivi karibuni, ripoti nchini Uingereza zinadai kuwa kocha mpya wa Chelsea, Xabi Alonso, anaweza kulazimika kumuuza mmoja wa mastaa wake msimu huu wa joto, huku dau la kuanzia kwa ajili ya Palmer likitajwa kuwa pauni milioni 80.
Kufuatia taarifa hizo, Neville amechambua faida ambazo United itazipata kama itafanikiwa kumnasa mchezaji huyo, akimlinganisha na sajili za kihistoria kama Rio Ferdinand, Wayne Rooney, na Roy Keane ambao walileta athari ya haraka klabuni hapo.
Akizungumza kupitia kipindi cha YouTube cha Rio Ferdinand, Neville alisema:
"Wakati Manchester United ilipomsajili Bryan Robson, Ron Atkinson alisema maneno kama 'hapa hakuna riski, hii ni dhahabu'. Nafikiri Harry Kane angekuwa usajili wa aina hiyo kwa United, huyo angekuwa dhahabu safi. Wewe [Ferdinand] ulipojiunga nasi ukitokea Leeds, Wazza [Rooney] akitokea Everton, na Roy Keane akitokea Nottingham Forest – hao wote walikuwa dhahabu."
Neville aliongeza kuwa Declan Rice pia alikuwa kwenye kundi hilo kabla ya kujiunga na Arsenal, akieleza kuwa wachezaji wa aina hiyo wanakuwa na uhakika wa kufanya vizuri kiasi kwamba mwishowe thamani yao inaonekana kuwa ndogo kulinganisha na mchango wao.
"Kama Sir Alex Ferguson angekuwa bado anaiongoza Man United, asingeruhusu kamwe Harry Kane kwenda klabu nyingine, angehakikisha anatua Old Trafford. Hali kadhalika kwa Declan Rice. Sir Alex angepigana kiume kuwapata wawili hao. Na si suala la kusajili wachezaji Waingereza tu, mwangalie hata Robin van Persie – alikuwa tayari amethibitisha uwezo wake kwenye Premier League na ulijua fika atakupa matokeo."
Neville Ana Wasiwasi na Uwezekano wa Dili Hilo
Ingawa Neville alivutiwa na biashara ya usajili iliyofanywa na United msimu uliopita, anaona kuwa nafasi ya kuwashawishi Chelsea kumuuza mchezaji kama Palmer ni ndogo sana, hata kukiwa na benchi jipya la ufundi chini ya Alonso.
Hungwe huyo wa zamani wa Old Trafford aliongeza:
"Nilipenda sajili za Matheus Cunha na Bryan Mbeumo msimu uliopita kwa sababu walikuwa tayari wamezoea mazingira ya Premier League. Hawakuwa 'dhahabu' ya moja kwa moja, lakini usajili wao ulikuwa na riski ndogo kwa sababu walikuwa tayari wamecheza ligi hii, walikuwa vijana wenye njaa ya mafanikio na walikuwa tayari kupanda daraja."
Neville alihitimisha kwa kusema:
"Aina hiyo ya sajili ni nzuri sana. Kuna mazungumzo kuhusu Cole Palmer na hilo linaonekana kama dili ambalo linaweza kuwa dhahabu kwa Manchester United kama akitua Old Trafford. Hata hivyo, sifikiri kama litatokea, naamini Chelsea watang'ang'ania kubaki naye. Lakini ukweli ni kwamba kuna wachezaji wachache sana wa aina hiyo sokoni, inachukua miaka mingi kupata fursa ya kumsajili mchezaji kama yeye."