Nyota wa klabu ya Motherwell, Elijah Just, ameng'ara kwa kufunga mabao mawili lakini timu yake ya New Zealand ilishindwa kulinda ushindi na kulazimishwa sare ya 2-2 na Iran katika mchezo wa Kombe la Dunia uliogubikwa na maandamano dhidi ya serikali ya Tehran.
Mchezo huo wa Kundi G uliopigwa kusini mwa jimbo la California ulikuwa na presha kubwa si tu uwanjani, bali hata majukwaani na nje ya uwanja kutokana na masuala ya kisiasa yanayoikabili nchi ya Iran.
Elijah Just Ang'ara, Iran Wajibu Mapigo
New Zealand ilianza mchezo huo kwa kasi na kupata bao la mapema kupitia kwa Elijah Just, aliyepiga shuti kali la 'volley' lililojaa wavuni baada ya kuandaliwa pasi safi na nahodha wake, Chris Wood.
Goli hilo lilishangiliwa kwa nguvu na baadhi ya mashabiki waliokuwa wakipinga serikali ya sasa ya Iran, huku wengi wao wakiwa wamebeba bendera za zamani za Iran zenye alama ya Simba na Jua (Lion and Sun). Aidha, baadhi ya mashabiki walizomea wimbo wa taifa wa Iran kabla ya mpira kuanza.
Hata hivyo, idadi kubwa ya mashabiki kwenye uwanja huo uliokusanya watu zaidi ya 70,000 walionekana kuwa nyuma ya timu yao ya taifa ('Team Melli'). Walisikika wakiimba kwa nguvu "Ir-ran! Ir-ran!" na uwanja ulilipuka kwa shangwe pale Ramin Rezaeian aliposawazisha goli hilo dakika chache baada ya nusu saa ya mchezo.
Rezaeian, ambaye ni miongoni mwa wachezaji kadhaa wa Iran ambao hawajacheza soka la klabu tangu mwezi Februari kutokana na kusimama kwa ligi yao ya ndani kufuatia mashambulizi ya anga ya Marekani na Israel, alionyesha ukakamavu wa haraka. Aliwahi mpira uliookolewa na mabeki na kumzidi ujanja mlinda mlango wa New Zealand aliyekuwa akitoka golini.
Mapema kipindi cha pili, ushirikiano wa Chris Wood na Just ulizaa matunda tena. Wood alipiga pasi ya upenyezi iliyomkuta Just, mwenye umri wa miaka 26, ambaye bila kupoteza muda alipiga shuti kali lililoipa All Whites uongozi wa mabao 2-1.
Lakini furaha ya New Zealand ilidumu kwa dakika 10 tu, kwani Iran walisawazisha tena kupitia goli safi la kichwa la Mohammad Mohebbi, aliyemalizia krosi safi ya Rezaeian na kufanya matokeo kuwa 2-2. Licha ya Iran kutengeneza nafasi nyingi nzuri kuelekea mwishoni mwa mchezo, walishindwa kupata bao la ushindi hadi filimbi ya mwisho inapulizwa.
Baada ya mechi, mfungaji wa goli la kwanza la Iran, Rezaeian, alifunguka kwa hisia:
"Nawapenda mama na baba yangu. Kila mara wananiombea katika nyakati ngumu, hivyo goli hili ni kwa ajili yao. Na pia ni kwa ajili ya watu wangu nchini Iran."
Hali ya Kundi G na Maoni ya Makocha
Matokeo haya yanamaanisha kuwa timu zote katika Kundi G sasa zina alama moja, baada ya Ubelgiji na Misri pia kutoka sare ya 1-1 mapema Jumatatu.
New Zealand, inayoshiriki fainali hizi kwa mara ya tatu, bado haijafanikiwa kupata ushindi kwenye Kombe la Dunia baada ya kucheza michezo saba sasa. Kwa upande wao, Iran inatafuta nafasi ya kutinga hatua ya mtoano kwa mara ya kwanza kabisa.
Kocha wa New Zealand, Darren Bazeley, alionyesha kusikitishwa na matokeo hayo:
"Tumesikitika kutoshinda mchezo huu. Unapoongoza mara mbili kwenye mchezo, unaondoka ukiwa unajiuliza ingekuwaje. Tulikuwa karibu sana kupata ushindi wetu wa kwanza wa Kombe la Dunia kuliko wakati mwingine woeote, lakini tulishindwa kulinda ushindi leo. Hata hivyo, tuko kwenye Kombe la Dunia, hatujapoteza, tumepambana, tumefunga mabao na kutengeneza nafasi. Ilikuwa kiwango bora sana ambacho ninajivunia."
Siasa na Maandamano Nje ya Uwanja
Mchezo huu ulionyesha wazi mgawanyiko mkubwa uliopo kati ya mashabiki wa Iran wanaoishi Marekani. Wengi wao walisema walikuwa na hisia msetoβkwa upande mmoja wakijivunia kuona nchi yao kwenye jukwaa kubwa la soka, na kwa upande mwingine wakiwa na hasira dhidi ya ukandamizaji wa serikali ya Tehran kwa waandamanaji, huku wakihofia pia mashambulizi ya mabomu ya Washington.
Jiji la Los Angeles lina idadi kubwa zaidi ya Wairani wanaoishi ughaibuni (diaspora), na kabla ya mechi kuanza, waandamanaji kati ya 300 hadi 500 walikusanyika nje ya uwanja wakipeperusha mabango na bendera kupinga serikali ya Tehran.
Hali ya maandalizi ya Iran pia haikuwa rahisi. Walilazimika kuhamisha kambi yao ya mazoezi kutoka Tucson, Arizona, na kwenda Tijuana, Mexico, ambako walipokelewa vizuri na wenyeji. Hata hivyo, mabadiliko hayo yanalazimisha kikosi hicho kusafiri safari za kimataifa kwa kila mechi ya makundi.
Kocha wa Iran, Amir Ghalenoei, alilalamika kuwa timu yake inalazimika kuruka usiku kurejea Mexico, huku akifichua kuwa rais wa shirikisho lao la soka pamoja na baadhi ya wasaidizi wake walinyimwa viza za kuingia Marekani.
"Nadhani labda timu yetu ndiyo inayodhulumiwa zaidi kwenye Kombe la Dunia," alisema Ghalenoei kupitia mkalimani wake.
Hata hivyo, alifurahishwa na mapokezi ya mashabiki uwanjani:
"Nadhani hali ya hewa ilikuwa nzuri sana uwanjani. Ilikuwa chanya sana, nilifurahi sana kuwaona mashabiki wakiwasuport wachezaji wa Iran. Nadhani hiyo ilikuwa mafanikio makubwa."
Katika michezo ijayo ya Kundi G siku ya Jumapili, Iran watarejea Los Angeles kukabiliana na Ubelgiji, wakati New Zealand watasafiri hadi Vancouver kumenyana na Misri.