Ujio wa Iraola na Mabadiliko Makubwa Anfield
Klabu ya Liverpool imeingia kwenye enzi mpya baada ya kumtangaza rasmi Andoni Iraola kuwa kocha mkuu mpya, akichukua mikoba ya Arne Slot. Iraola, ambaye mkataba wake na Bournemouth umefikia kikomo, ameeleza kufurahishwa kwake na nafasi hiyo ya kuinoa timu hiyo yenye historia kubwa duniani.
Hata hivyo, mashabiki wa 'Majogoo wa Merseyside' wanapaswa kujiandaa kwa mabadiliko makubwa kwenye kikosi chao msimu huu wa joto. Ripoti za hivi punde zinaashiria kuwa kocha huyo raia wa Uhispania anaweza kufanya usafishaji mkubwa wa kikosi, huku hadi wachezaji wanane wakitajwa kuwa kwenye hatari ya kuondoka Anfield.
Iraola Azuia Dili la Alisson Kwenda Juventus
Moja ya maamuzi makubwa ya kwanza ya Iraola ni pamoja na kuzuia kuondoka kwa mlinda mlango tegemeo, Alisson Becker. Kabla ya kuteuliwa kwa Iraola, kulikuwa na tetesi kali zilizomhusisha Mbrazil huyo na miamba ya Serie A, Juventus.
Hata hivyo, kwa mujibu wa jarida la michezo la nchini Italia, Gazzetta Dello Sport, Iraola hana mpango wowote wa kumruhusu Alisson kuondoka. Kocha huyo mpya anataka Alisson asalie kuwa kipa wake namba moja kwa msimu ujao.
"Alisson atajaribu kuwasiliana na uongozi wa Liverpool tena katika saa chache zijazo ili kupata baraka zao za kuondoka, lakini kwa sasa Juventus wanashikilia matumaini tu bila uhakika wowote. Na tayari wameanza kuangalia mbadala mwingine,"- liliripoti jarida hilo.
Kutokana na msimamo huo mkali wa Iraola, Juventus sasa wamehamishia nguvu zao kwa kipa wa Aston Villa, Emiliano Martinez, pamoja na mlinda mlango wa Tottenham, Guglielmo Vicario.
Hatima ya Mamardashvili na Wachezaji Wengine Hatarini
Ikiwa Alisson atasalia Anfield kama Iraola annavyotaka, hatua hiyo itakuwa na athari kwa makipa wengine klabuni hapo. Giorgi Mamardashvili, ambaye alisajiliwa msimu uliopita akitokea Valencia, anaweza kujikuta akilazimika kuondoka kwa mkopo au kuuzwa ili kupata nafasi ya kucheza mara kwa mara.
Mbali na Alisson na Mamardashvili, tayari imethibitishwa kuwa nyota watatu wa kikosi cha kwanza—Andy Robertson, Ibrahima Konate, na Mohamed Salah—wataondoka klabuni hapo msimu huu wa joto. Hili linaacha mapengo makubwa ambayo Iraola atalazimika kuyaziba haraka.
Kwa mujibu wa ripoti kutoka Liverpool.com, kuna orodha ya wachezaji wengine sita ambao mustakabali wao upo shakani chini ya utawala wa kocha huyu mpya. Wachezaji hao ni pamoja na:
- Curtis Jones
- Harvey Elliott
- Joe Gomez
- Alexis Mac Allister
- Wataru Endo
- Federico Chiesa
Wachezaji hawa watatakiwa kumthibitishia Iraola wakati wa maandalizi ya msimu mpya (pre-season) kwamba wanastahili nafasi kwenye mfumo wake wa uchezaji, la sivyo milango ya kutokea ipo wazi.
Iraola Afunguka Msisimko Wake Kujiunga na Liverpool
Akizungumza na vyombo vya habari vya klabu hiyo baada ya kutangazwa rasmi siku ya Alhamisi jioni, Iraola hakuficha hisia zake juu ya ukubwa wa changamoto iliyo mbele yake:
"Nna msisimko mkubwa sana, msisimko wa kweli. Kila mtu anaijua Liverpool, unajua ni klabu kubwa, klabu kubwa sana, moja ya kubwa zaidi duniani. Lakini kuwa hapa ndani na kuanza kuielewa klabu hii kidogo, kila mara nimekuwa nikiamini kuwa hii ni klabu ya pekee."
Aliongeza kuwa kuvutiwa na Liverpool hakuhitaji mambo mengi kwa sababu jina la klabu hiyo pekee linajieleza yenyewe:
"Huitaji mambo mengi ili kuvutiwa na Liverpool. Liverpool ni Liverpool. Lakini kipekee, mazingira ya hapa, mashabiki, klabu, wachezaji, na fursa ya mimi kufundisha wachezaji wa kiwango cha juu duniani, pamoja na kupigania mataji. Nafikiri hakuna kitu chenye mvuto zaidi ya hiki. Ni ngumu kukipata kwingineko. Hivyo basi, nina hamu kubwa ya kuanza kazi."
Mashabiki wa Liverpool sasa wanasubiri kwa hamu kuona jinsi Iraola atakavyosuka kikosi chake kipya huku kukiwa na ripoti kuwa makubaliano ya usajili wa wachezaji wake wawili wa kwanza tayari yamefikia hatua nzuri.