Mabingwa wa soka nchini Uingereza, Manchester City, wamepata ushindi mkubwa nje ya uwanja baada ya kufikia makubaliano ya kumpa mkataba mpya wa muda mrefu beki wao tegemeo wa kimataifa wa Croatia, Josko Gvardiol. Hatua hii inakuja kama ngao thabiti dhidi ya miamba ya Hispania, Real Madrid na Barcelona, ambao walikuwa wakinyemelea saini ya nyota huyo.
Mtaalamu wa masuala ya uhamisho wa wachezaji duniani, Fabrizio Romano, amethibitisha kuwa dili hilo sasa limekamilika na Gvardiol ataendelea kusalia Etihad kwa miaka mingi ijayo.
Gvardiol Kupiga Saini Hadi Juni 2031
Manchester City walitunisha misuli na kushinda vita dhidi ya klabu kubwa za Ulaya mnamo mwaka 2023 walipomsajili Gvardiol kutoka RB Leipzig kwa ada iliyokadiriwa kuwa pauni milioni 77. Tangu wakati huo, beki huyo mwenye umri wa miaka 24 amekuwa muhimili mkubwa kwenye safu ya ulinzi.
Chini ya aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Pep Guardiola, Gvardiol hakung'ara tu kama beki wa kati, bali pia alicheza kwa kiwango cha juu sana kama beki wa kushoto. Licha ya msimu wa 2024/25 kuwa mzuri sana kwake, majeraha yalitatiza kasi yake msimu huu na kumfanya acheze mechi 18 tu za Ligi Kuu ya Uingereza (Premier League), jambo lililochochea tetesi za yeye kutaka kutimkia Real Madrid.
Hata hivyo, Fabrizio Romano kupitia ukurasa wake wa X (zamani Twitter) ameweka wazi kuwa Gvardiol ameshajifunga rasmi klabuni hapo.
"BREAKING: Dili la Joško Gvardiol limekamilika na kuthibitishwa baada ya kusaini mkataba mpya na Manchester City. Makubaliano ni hadi Juni 2031 na mpango wa kwenda Hispania msimu huu wa joto umezimika rasmi. Anaonekana kama mchezaji muhimu sana na mkurugenzi Hugo Viana pamoja na kocha mpya Enzo Maresca."
Mwandishi wa habari za michezo kutoka Ujerumani, Florian Plettenberg, pia amethibitisha habari hizo akieleza kuwa masuala yote muhimu yameshakamilika na kilichobaki ni kutangazwa tu rasmi.
Kwa Nini Kubaki kwa Gvardiol ni Ushindi Mkubwa kwa City?
Kuondoka kwa baadhi ya nguzo muhimu klabuni hapo kulileta wasiwasi mkubwa kwa mashabiki wa Man City. Romano alifafanua umuhimu wa kumpiga pingu Gvardiol katika kipindi hiki cha mpito cha klabu hiyo:
"Pep Guardiola ameondoka. John Stones ameondoka. Bernardo Silva naye ameondoka. Kupoteza mchezaji mwingine tegemeo lingekuwa pigo kubwa sana kwa klabu. Kulikuwa na nia thabiti kutoka Real Madrid na Barcelona, lakini sasa City wanatarajia mchezaji huyo kubaki."
Chini ya uongozi mpya wa kocha Enzo Maresca, Gvardiol anatazamwa kama nguzo kuu ya ujenzi wa kikosi kipya kitakachoendeleza utawala wa City kwenye soka la Uingereza na Ulaya.
Hatma ya Enzo Fernandez Kujiunga na Man City
Wakati City wakisherehekea kumbakiza Gvardiol, upande wa usajili mpya kuna ripoti kuhusu kiungo wa Chelsea, Enzo Fernandez. Nyota huyo wa kimataifa wa Argentina amekuwa akihusishwa mara kwa mara na kutaka kuhamia Manchester City ili kuungana tena na kocha wake wa zamani, Enzo Maresca.
Hata hivyo, ripoti kutoka kwa mwandishi wa BBC Sport, Nizaar Kinsella, zinaeleza kuwa Man City pamoja na Paris Saint-Germain wamejiondoa kwenye mbio hizo za kuwania saini yake, na sasa Fernandez ana macho yake kwenye klabu moja tu.
Ripoti hiyo inasema:
"Vyanzo vya kuaminika vinasema Fernandez ana nia ya dhati ya kuondoka Chelsea na kujiunga na Real Madrid. Manchester City na Paris St-Germain walikuwa wakihusishwa naye, lakini inaeleweka kuwa vilabu vyote viwili vimejitenga na nia hiyo. Inaonekana sasa ni Real Madrid au hakuna kitu kwa Fernandez."
Licha ya nia yake hiyo ya kutaka kwenda Santiago Bernabeu, Chelsea—ambayo sasa ipo chini ya kocha mpya Xabi Alonso—itakuwa tayari kuendelea kubaki na kiungo huyo aliyefunga mabao 15 na kutoa pasi za mabao 7 msimu uliopita. Fernandez ana mkataba wa muda mrefu na Chelsea unaoishia mwaka 2032, jambo linalofanya uhamisho wake kuwa mgumu isipokuwa tu kama Real Madrid watatoa ofa ya kufuru.