USAJILI 2026-06-14 3 min read

Usajili wa Kwanza Man United Waiva: Ederson Kufanya Vipimo vya Afya Leo, Kinda wa Newcastle Naye Awashika Sikio

Manchester United inakaribia kukamilisha usajili wake wa kwanza wa majira ya joto huku ripoti zikitaja kuwa kiungo wa Atalanta, Ederson, anafanyiwa vipimo vya afya leo mjini New York, huku wakimvizia pia Lewis Hall wa Newcastle.

Usajili wa Kwanza Man United Waiva: Ederson Kufanya Vipimo vya Afya Leo, Kinda wa Newcastle Naye Awashika Sikio
#manchesterunited #ederson #lewishall #newcastleunited #atalanta #usajili

Manchester United inakaribia kukamilisha usajili wake wa kwanza wa majira ya joto huku ripoti zikitaja kuwa dili la kiungo wa Atalanta, Ederson, liko kwenye hatua za mwisho. Wakati huohuo, klabu hiyo bado inaendelea kupambana chini kwa chini kupata saini ya beki wa kushoto wa Newcastle United, Lewis Hall.

Taarifa nyingi kutoka barani Ulaya zimeeleza kuwa Mashetani Wekundu tayari walishamaliza makubaliano ya kumsajili Ederson tangu mapema, lakini ushiriki wake kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Brazil ulikuwa ukichelewesha kukamilika kwa dili hilo rasmi.

Ederson Kufanya Vipimo vya Afya Leo New York

Gazeti maarufu la michezo la nchini Italia, Corriere Dello Sport, limefichua kuwa kiungo huyo mkata umeme hatimaye anafanya vipimo vya afya leo Jumapili huko New York, Marekani.

Taarifa hiyo iliyotolewa mwishoni mwa wiki ilieleza:

"Ederson kwenda United, mambo tayari. Baada ya mchezo dhidi ya Morocco, kiungo huyo wa Brazil atafanyiwa vipimo vya afya mjini New York kwa ajili ya uhamisho wake kwenda Manchester United, na baada ya hapo atakuwa huru kusaini mkataba rasmi na klabu hiyo ya Uingereza."

Gazeti hilo liliongeza kuwa dili hilo lina thamani ya euro milioni 45 kwenda Atalanta, makubaliano ambayo yalifikiwa karibu mwezi mmoja uliopita huku United wakiwapiku Atletico Madrid waliokuwa wakimnyatia mchezaji huyo. Nyota huyo aliyezaliwa mwaka 1999 ameitwa kwenye kikosi cha Brazil na kocha Carlo Ancelotti kuchukua nafasi ya Wesley aliyepata majeraha, na kwa sasa yuko kwenye majukumu ya Kombe la Dunia na timu yake ya taifa (Selecao).

Ingawa usajili wa Ederson unaonekana kukamilika, Man United haina mpango wa kuishia hapo. Miamba hiyo ya Old Trafford inatajwa kusaka kiungo mwingine mmoja zaidi, beki wa kushoto, pamoja na winga wa kushoto. Vilevile, kuna tetesi kuwa wanaweza kuongeza bajeti yao ili kusajili beki wa kati na mshambuliaji mpya.

Lewis Hall Kichwani mwa Mabosi wa Old Trafford

Beki wa kushoto wa Newcastle United, Lewis Hall, ni miongoni mwa wachezaji wanaohusishwa vikali na uhamisho wa kwenda Old Trafford. Mtaalamu wa masuala ya usajili, Fabrizio Romano, amethibitisha kuwa Manchester United imeendelea kuweka mawasiliano hai na watu wa karibu wa mchezaji huyo.

Akizungumza kupitia chaneli yake ya YouTube, Romano alisema:

"Nilitaka kupenyeza neno kuhusu Manchester United, kwa sababu katika siku mbili au tatu zilizopita, klabu hiyo imekuwa ikiwasiliana mara kwa mara na watu wa karibu wa Lewis Hall, beki wa kushoto wa Newcastle."

Romano aliongeza kuwa United ilionyesha nia ya dhati tangu wiki chache zilizopita na wanamhusudu sana mchezaji huyo:

"Manchester United tayari ilifanya mawasiliano wiki chache zilizopita. Wana nia ya kweli na mchezaji huyu. Wanampenda sana Lewis Hall, hivyo ni mmoja wa wachezaji wanaowawinda. Tunajua kuwa watakuwa na kazi kubwa kwenye eneo la viungo, eneo ambalo linapewa kipaumbele kwa sasa kwani dili la Ederson tayari limeshakamilika."

Romano alihitimisha kwa kueleza kuwa baada ya Ederson kutua rasmi, kiungo mwingine mmoja au wawili wanaweza kufuata, kisha nguvu kubwa itaelekezwa kwenye nafasi ya beki wa kushoto ambapo Lewis Hall ndiye anayeongoza kwenye orodha ya wanaotakiwa.

© 2026 Mkeka wa Leo
Haki zote zimehifadhiwa