Man Utd Yajiandaa Kupindua Meza Kupata Saini ya Summerville
Mambo yanaonekana kupamba moto huko Old Trafford. Manchester United wameripotiwa kutuma 'ofa nzito' kwa ajili ya kumsajili nyota wa West Ham United, Crysencio Summerville, kufuatia taarifa za mwandishi nguli wa habari za michezo, David Ornstein, aliyefichua nia ya klabu hiyo.
Summerville alionja machungu ya kushuka daraja na West Ham mwishoni mwa msimu wa 2025/26, lakini kiwango chake binafsi kimekuwa bora sana katika miezi ya hivi karibuni. Winga huyo machachari alikuwa mmoja wa wachezaji tegemeo wa Wagonga Nyundo hao wa London katika mechi za lala-salama, na hivi karibuni aling'ara akiifungia Uholanzi bao safi kabisa katika mchezo wao wa kwanza wa hatua ya makundi ya Kombe la Dunia.
Kiwango hiki kimevutia klabu kadhaa za Ligi Kuu ya Uingereza (Premier League), na kwa sasa ni vigumu kumuona winga huyo akisalia West Ham msimu ujao.
David Ornstein Afichua Masharti Mawili ya INEOS
Ingawa Tottenham Hotspur wamekuwa wakihusishwa na Summerville, Ornstein amebainisha kuwa Manchester United ndio klabu ya kuitazama zaidi kwa sasa. Hata hivyo, dili hili halitakuwa rahisi kwani linategemea mambo mawili makuu.
Kwanza kabisa, Man Utd wanatakiwa kufikia dau la West Ham linalokadiriwa kuwa pauni milioni 50 ili kuishawishi klabu hiyo kumwachia mchezaji huyo ambaye mkataba wake unamalizika Juni 2029.
Pili, usajili huu utategemea sana hatomstakabali wa Marcus Rashford huko Old Trafford. Ripoti kutoka The Athletic zinaeleza:
'Miongoni mwa klabu zinazofuatilia kwa karibu hali ya Summerville ni Manchester United, huku winga huyo msumbufu akiwa miongoni mwa machaguo makuu yanayofikiriwa iwapo watasajili katika nafasi hiyo. United wameulizia kuhusu hali yake na wanafahamu kuwa inatarajiwa kugharimu takriban pauni milioni 50 kwa West Ham kuruhusu kuondoka kwa mchezaji huyo ambaye ana mkataba hadi Juni 2029.'
Ripoti hiyo iliongeza kuwa hatua hiyo inahusishwa moja kwa moja na kile kitakachomtokea Rashford:
'Mengi yatategemea mustakabali wa Marcus Rashford, ikizingatiwa kwamba Barcelona hawakutumia kipengele cha kumnunua cha euro milioni 30 baada ya mkataba wake wa mkopo wa msimu mzima kumalizika hivi karibuni.'
Ofa ya Euro Milioni 60 Mezani
Wakati masuala ya Rashford yakijadiliwa, ripoti kutoka nchini Uhispania kupitia mtandao wa Fichajes zinadai kuwa Summerville amekuwa 'shabaha kuu' ya Man Utd, na mashetani hao wekundu tayari wameweka ofa kubwa mezani ili kuwawahi wapinzani wao.
Mtandao huo unaamini kuwa United ndio wanaopewa nafasi kubwa zaidi ya kunasa saini ya mchezaji huyo kwa sasa:
'Winga huyo wa Kiholanzi mwenye umri wa miaka 24 anatarajiwa kuondoka West Ham kufuatia klabu hiyo ya London kushuka daraja hadi Championship. Kwa sasa akiwa na timu yake ya taifa kwenye Kombe la Dunia, winga huyo ni mmoja wa wachezaji wanaowindwa sana katika soko la usajili. Old Trafford sasa inaonekana kuwa mstari wa mbele kupata huduma yake. Ofa ya awali inaweza kuwa karibu euro milioni 60, ingawa West Ham hawajatupilia mbali uwezekano wa kudai kiasi kikubwa zaidi kwa mmoja wa wachezaji wao wenye kasi na ushawishi mkubwa.'
Kuboresha Kikosi kwa ajili ya Klabu Bingwa Ulaya
Kwa sasa, vipaumbele vya usajili vya Manchester United vipo kwenye eneo la kiungo ambapo wanatafuta mabadiliko makubwa chini ya uongozi wa INEOS. Baada ya kukamilisha dili la Ederson Silva, Matheus Fernandes wa West Ham anatajwa kuwa anayefuata.
Hata hivyo, klabu hiyo inataka kuongeza nguvu katika maeneo mengine ili kuwa na kikosi kipana na chenye ushindani watakaporudi kwenye michuano ya Klabu Bingwa Ulaya (Champions League) msimu ujao. Eneo la winga wa kushoto ni moja ya maeneo yanayopewa kipaumbele, na Summerville anatajwa kuwa mtu sahihi wa kuleta chachu mpya ya ushindani kikosini.