TETESI ZA USAJILI 2026-06-06 3 min read

Man Utd 'Wapewa Nafasi Kubwa' Kumsajili Tonali, Waandaa Pauni Milioni 80

Manchester United wanaripotiwa kuwa mstari wa mbele kumnasa kiungo wa Newcastle United, Sandro Tonali, wakijiandaa kutoa ofa ya pauni milioni 80 msimu huu wa joto.

Man Utd 'Wapewa Nafasi Kubwa' Kumsajili Tonali, Waandaa Pauni Milioni 80
#manchesterunited #newcastleunited #sandrotonali #tetesizausajili #premierleague

Carrick Ataka Kukiwasha: Tonali Ndiye Target Namba Moja

Klabu ya Manchester United imeanza mikakati thabiti ya kukisuka upya kikosi chake chini ya meneja mpya wa kudumu, Michael Carrick. Baada ya kumaliza msimu wa 2025/26 kwa kishindo kwa kushika nafasi ya tatu na kukata tiketi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, Carrick anakabiliwa na kibarua kizito cha kuimarisha maeneo kadhaa kikosini ili kuhimili mikikimikiki ya michuano mbalimbali msimu ujao.

Taarifa mpya zinasema kuwa kipaumbele kikuu cha Mashetani Wekundu kwa sasa ni kuifanyia marekebisho makubwa safu yao ya kiungo. Huku Manuel Ugarte akitarajiwa kufuata nyayo za Casemiro kuondoka Old Trafford msimu huu wa joto, United inajiandaa kusajili viungo wapya watatu. Tayari wameshakamilisha usajili wa nyota wa Atalanta, Ederson Silva, na sasa macho yote yamehamia kwa Sandro Tonali wa Newcastle United.

Sababu za Tonali Kutaka Kuondoka Newcastle

Sandro Tonali amekuwa mmoja wa viungo bora zaidi barani Ulaya na uwezo wake umevutia klabu nyingi kubwa. Hata hivyo, Newcastle United wanalazimika kufanya maamuzi magumu ya kuuza baadhi ya wachezaji wao nyota ili kusawazisha mahesabu yao ya kifedha, hasa baada ya kufeli kufuzu michuano ya Ulaya msimu huu. Hata baada ya kumuuza Anthony Gordon, bado miamba hiyo ya St James' Park inahitaji kupata pesa zaidi ili kuepuka rungu la sheria za kifedha.

Ingawa klabu kama Arsenal na Manchester City zimeonyesha nia ya kumtaka Tonali, ripoti kutoka kwa mwandishi wa habari Mark Brus kupitia Caught Offside zinaeleza kuwa klabu hizo kwa sasa zina vipaumbele vingine. Hali hii inaipa Manchester United nafasi kubwa ya kuwa 'favorites' wa kumnasa kiungo huyo wa kimataifa wa Italia.

Vuta Nikuvute ya Dau la Usajili

Manchester United wanaripotiwa kuwa tayari kuwasilisha ofa ya kwanza ya kiasi cha pauni milioni 70 hadi milioni 80 ili kumpata Tonali. Hata hivyo, dili hili halitakuwa rahisi kwani Newcastle wameweka msimamo mkali kuhusu thamani ya mchezaji huyo.

Chanzo cha habari cha Caught Offside kimeeleza hivi:

"Manchester United na kampuni ya INEOS wapo kwenye ukurasa mmoja – baada ya kukamilisha usajili wa Ederson, sasa wapo tayari kumgeukia Tonali. Newcastle hawataki kumuuza, na watashikilia msimamo wa kutaka angalau pauni milioni 100. Hata hivyo, United hawawezi na hawatakuwa tayari kulipa kiasi hicho, hivyo wanatarajiwa kupima upepo kwa ofa ya kwanza ya karibu pauni milioni 70 hadi 80."

Mapinduzi ya Viungo Pale Old Trafford

Mbali na Tonali, United pia inahusishwa kwa karibu na kiungo wa West Ham, Matheus Fernandes, na kuna imani kubwa ndani ya klabu kuwa dili hilo linaweza kukamilika hivi karibuni. Mpango wa INEOS ni kuhakikisha Carrick anakuwa na safu ya kiungo yenye nguvu, kasi, na ubunifu mkubwa ili kupambana kikamilifu kwenye Ligi Kuu ya Uingereza na Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao. Mashabiki wa United sasa wanasubiri kuona kama uongozi wao utafanikiwa kuvunja ukuta wa Newcastle na kumleta Tonali huko Old Trafford.

© 2026 Mkeka wa Leo
Haki zote zimehifadhiwa