Mpango wa 'Galactico' Mpya Kupitia Florentino Perez
Rais wa Real Madrid, Florentino Perez, anajipanga kuvunja rekodi ya usajili ya klabu hiyo kwa ajili ya kumnasa winga wa Paris Saint-Germain, Khvicha Kvaratskhelia. Ripoti mpya zinaeleza kuwa nyota huyo wa kimataifa wa Georgia yuko tayari kujiunga na miamba hiyo ya Estadio Bernabeu msimu huu wa kiangazi.
Perez alilipua bomu la habari wiki hii wakati akieleza mpango wake wa kushusha mchezaji mwenye hadhi ya 'Galactico' katika dirisha linalokuja la usajili. Wakati akijiaandaa na uchaguzi mkuu wa urais wa Real Madrid, kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 79 ana uhakika mkubwa wa kuibuka na ushindi na tayari ameanza kusuka dandi lake la nguvu.
Akizungumza kuhusu usajili huo wa siri, Perez alisema:
"Hivi karibuni, siku ya Jumanne, nitaenda kutoa ofa kwa klabu inayocheza Ligi ya Mabingwa Ulaya, ambayo itakuwa ndiyo malipo makubwa zaidi kuwahi kufanywa na Real Madrid kwa mchezaji katika historia yao, angalau Euro milioni 150."
"Sio [Jeremy] Doku, sio [Erling] Haaland, sio [Harry] Kane, na wala sio [Michael] Olise... Ofa hii ya Euro milioni 150 sio kwa ajili ya beki. Inaweza kuwa kiungo au mshambuliaji. Ni mchezaji kijana na hatoki Ligi Kuu ya Uingereza (Premier League). Ni Galactico wa kweli."
Mkanganyiko wa Tetesi: Je, ni Olise, Vitinha au Kvaratskhelia?
Kauli hiyo ya Perez ilizua taharuki na gumzo kubwa barani Ulaya kuhusu mchezaji gani anayezungumziwa. Baadhi ya vyombo vya habari nchini Ureno, kama vile gazeti la Record, vilidai kuwa Perez alikuwa anamzungumzia kiungo wa PSG, Vitinha.
Kwa upande mwingine, mtaalamu wa usajili Fabrizio Romano na gazeti la The Telegraph waliripoti kuwa mchezaji anayewindwa ni winga wa Bayern Munich na timu ya taifa ya Ufaransa, Michael Olise. Romano alifichua kuwa vyanzo vya ndani vya Real Madrid vilibainisha kuwa Perez alikuwa anapiga chenga za maneno (bluffing) ili asiharibu mambo mapema.
Kulingana na Romano, Perez anavutiwa mno na Olise kutokana na kiwango alichokionyesha kwenye mechi za Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu dhidi ya Real Madrid, na anaamini mchezaji huyo angefaa sana kwenye mfumo wa Jose Mourinho hapo Bernabeu ili kuunda safu hatari zaidi ya ushambulizi duniani akishirikiana na Kylian Mbappe na Vinicius Junior.
Ukweli Wafichuka: Kvaratskhelia ndiye 'Target' wa Madrid
Hata hivyo, taarifa za hivi punde kutoka chombo cha habari cha kuaminika cha TEAMtalk zimefichua kuwa mchezaji ambaye Perez anamnyemelea kwa dau hilo la Euro milioni 150 si mwingine bali ni winga wa Paris Saint-Germain, Khvicha Kvaratskhelia.
Inaripotiwa kuwa Real Madrid wanajiandaa kuwasilisha ofa hiyo rasmi wiki ijayo. Mazungumzo ya awali tayari yamefanyika chini kwa chini, na uongozi wa Los Blancos una amani ya kutosha ukiamini kuwa winga huyo mwenye umri wa miaka 25 angependa kuhamia katika mji mkuu wa Uhispania.
Chanzo cha karibu na Real Madrid kimeeleza:
"Vyanzo vilivyo karibu na Real Madrid vimetuthibitishia kuwa Kvaratskhelia ndiye mchezaji anayejadiliwa ndani ya klabu na kwamba kazi ya msingi ya kuanzisha mchakato huo tayari imefanyika. Kuna imani kubwa miongoni mwa vigogo wa Madrid kuwa mchezaji huyo yuko tayari kwa changamoto hiyo mpya."
Kibarua Kizito Kuishawishi PSG
Hata hivyo, dili hili halitakuwa rahisi hata kidogo. PSG hawana nia ya kumuuza Kvaratskhelia, jambo ambalo linafanya mazungumzo na mabingwa hao wa Ulaya kuwa magumu na yenye kuhitaji mbinu za hali ya juu.
Kvaratskhelia alijiunga na PSG akitokea Napoli mnamo Januari 2025. Tangu wakati huo, amekuwa nguzo muhimu akifunga mabao 27 na kutoa pasi za mabao (assists) 19 katika michezo 80 aliyoichezea klabu hiyo ya Ufaransa. Akiwa na uwezo wa kucheza winga zote mbili, kulia na kushoto, Kvaratskhelia ameshatwaa mataji mawili ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na taji la Ligue 1 akiwa na PSG, mbali na mataji mawili ya Serie A aliyotwaa zamani akiwa na Napoli.