Mtaalamu wa masuala ya usajili barani Ulaya, Fabrizio Romano, amefichua kuwa kocha anayetarajiwa kutua Real Madrid, Jose Mourinho, anatamani mno saini za viungo wa Paris Saint-Germain, Joao Neves na Vitinha.
Mourinho anapewa nafasi kubwa ya kurejea kikosini hapo iwapo Florentino Perez atashinda uchaguzi wa urais wa klabu hiyo unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa wiki hii. Kocha huyo Mreno aliwahi kukinoa kikosi cha miamba hiyo ya Hispania kati ya mwaka 2010 na 2013, ambapo alitwaa mataji matatu makubwa ikiwemo taji la La Liga.
Tayari Real Madrid imeshajihakikishia saini za beki Ibrahima Konate na Denzel Dumfries, huku rais wa sasa Florentino Perez akipanga kumpatia Mourinho kikosi chenye ushindani mkubwa msimu ujao.
Ndoto ya Perez na Mourinho Kumsajili Joao Neves na Vitinha
Kulingana na Romano, Mourinho angependa kuungana na Wareno wenzake, Joao Neves na Vitinha, ndani ya Santiago Bernabeu. Mwandishi huyo wa habari kutoka nchini Italia ameeleza kuwa hata Perez mwenyewe anavutiwa mno na viungo hao wa kimataifa wa Ureno, ambao wamekuwa nguzo muhimu katika mafanikio ya PSG ya kutwaa mataji ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mfululizo.
Vitinha alijiunga na PSG akitokea FC Porto msimu wa joto wa mwaka 2022 kwa dau la euro milioni 40, huku Neves akisajiliwa kutoka Benfica msimu wa joto wa mwaka 2024 kwa dau la euro milioni 60.
Hata hivyo, ingawa Real Madrid inatamani saini za nyota hao, Romano ameweka wazi kuwa PSG haina mpango kabisa wa kuwauza kwenye dirisha hili la usajili.
Akiizungumzia hali hiyo kupitia chaneli yake ya YouTube, Romano alisema:
"Ni muhimu kusema hili kwa sababu wengi wenu mnauliza kwa nini isiwe Vitinha, kwa nini isiwe Joao Neves? Hawa ni wachezaji wawili ambao wanabaki kabisa kwenye orodha ya ndoto ya Florentino Perez. Ni wachezaji ambao Florentino Perez anawapenda sana. Hawa ni wachezaji wawili wa Kireno, na Jose Mourinho pia anawapenda sana."
Romano aliongeza kuwa Jose Mourinho pia anavutiwa nao mno, lakini akasisitiza kuwa mlango wa PSG kufanya biashara umefungwa kwa sasa:
"Kwa sasa, uelewa wangu ni kwamba mlango wa Paris Saint-Germain kuruhusu mchezaji yeyote kati ya hawa kuondoka hauhusiani na pesa. PSG haitaki kabisa kuwauza wachezaji hawa. Wanataka kuendelea na kikosi hiki hiki, labda Goncalo Ramos anaweza kuondoka, Chevalier anaweza kuondoka, Kang-in Lee anaweza kuondoka, lakini kwa ujumla, wanataka kikosi chao cha kwanza kibaki kile kile ili msimu ujao wajaribu tena kubeba Ligi ya Mabingwa na kuandika historia ya kutwaa mataji matatu mfululizo. Hiyo ndiyo dhamira ya Paris Saint-Germain."
Mtego wa Euro Milioni 150 kwa Michael Olise
Katika hatua nyingine, Romano amefichua kuwa Rais wa Real Madrid, Florentino Perez, anapanga kuwasilisha ofa kubwa ya euro milioni 150 kwa ajili ya winga wa Bayern Munich na timu ya taifa ya Ufaransa, Michael Olise.
Hivi karibuni, Perez alikiri kuwa anapanga kufanya ofa ya kihistoria kwa mmoja wa wachezaji bora duniani lakini alikanusha kuwa mchezaji huyo ni Olise. Perez alisema:
"Nitafanya ofa hivi karibuni kwa klabu inayocheza Ligi ya Mabingwa, siku ya Jumanne, ambayo itakuwa ofa kubwa zaidi ambayo Real Madrid haijawahi kuifanya kwa mchezaji yeyote katika historia yake, angalau euro milioni 150. Sio Jeremy Doku, sio Erling Haaland, sio Harry Kane, na wala sio Michael Olise... Ofa hii ya euro milioni 150 sio kwa ajili ya beki. Anaweza kuwa kiungo au mshambuliaji, ni mchezaji mdogo na hatokei Ligi Kuu ya Uingereza. Ni 'Galactico' wa kweli."
Hata hivyo, Romano ameweka wazi kuwa Perez alikuwa anapiga chenga za jukwaani ili kuficha mipango yake:
"Vyanzo vya ndani kutoka Real Madrid vinahakikisha kuwa Florentino alikuwa anadanganya. Hakutaka kutaja jina la mchezaji huyo kabla ya kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na klabu husika. Hakutaka kusema lolote hadharani ili asionekane kama mgombea mwingine, Enrique Riquelme, ambaye saa 24 kabla alikuwa akionyesha jezi ya Erling Haaland na kumtangaza kama usajili wake mtarajiwa."
Kulingana na Romano, Perez alizama kwenye vilindi vya mahaba ya soka la Olise wakati wa michezo ya Ligi ya Mabingwa kati ya Bayern Munich na Real Madrid msimu huu. Perez anaamini kuwa mfumo ambao Jose Mourinho anataka kuutumia Real Madrid utakuwa bora zaidi ukiwa na mchezaji huyo wa Kifaransa, akiamini kuwa safu ya ushambuliaji itakayoundwa na Kylian Mbappe, Vinicius Junior, na Michael Olise itakuwa tishio kubwa zaidi duniani.