Mshambuliaji wa zamani na gwiji wa soka wa Ufaransa na klabu ya Arsenal, Thierry Henry, ametabiri timu atakazoziangazia zaidi kwenye fainali za Kombe la Dunia. Henry ameitaja nchi yake ya Ufaransa kama timu inayopewa nafasi kubwa zaidi ya kutwaa ubingwa huo, huku akizitaja nchi mbili ambazo zinaweza kuleta upinzani wa kushtukiza (dark horses) kwenye michuano hiyo mikubwa zaidi ya soka duniani.
Henry, ambaye alitwaa Kombe la Dunia akiwa na Ufaransa mwaka 1998, anaamini kuwa kikosi cha 'Les Bleus' kina kila kitu kinachohitajika ili kurudia mafanikio hayo. Ufaransa walitwaa ubingwa huo mwaka 2018 nchini Urusi kwa kuifunga Croatia, kabla ya kupoteza kwa penalti dhidi ya Argentina kwenye fainali ya kusisimua ya mwaka 2022 nchini Qatar.
Mataifa Matano Yanayopewa Nafasi Kubwa na Henry
Katika mahojiano yake na jarida la Sports Illustrated, Henry aliitaja Ufaransa kama chaguo lake la kwanza lakini hakuacha nyuma mataifa mengine makubwa yenye vikosi vyenye vipaji vya hali ya juu.
"Naiona Ufaransa kama timu inayopewa nafasi kubwa zaidi – kwa sehemu fulani ni kwa sababu mimi ni Mfaransa, lakini pia kwa sababu tumefika fainali mbili zilizopita," alisema Henry.
Mbali na Ufaransa, Henry alitaja mataifa mengine manne ambayo anaona yana nafasi kubwa ya kufanya vizuri na kupigania ubingwa huo:
"Tuna timu imara. Uhispania, Argentina, Ureno, na Uingereza nazo pia ni timu zenye matumaini makubwa. Lakini mambo ya kushangaza kutoka kwa timu kama Norway au Senegal yanaweza kutokea."
Kutajwa kwa Senegal na Norway kumeweka gumzo kubwa, kwani timu hizi mbili hazijazoeleka kuwekwa kwenye kundi la timu zinazoweza kutishia mataifa makubwa kwenye hatua za mwisho za Kombe la Dunia.
Brazil na Ujerumani Kutoonekana Kwenye Orodha ya Henry
Moja ya mambo yaliyoshangaza wengi ni Henry kutoitaja Brazil, ambayo ndiyo nchi yenye mafanikio makubwa zaidi katika historia ya Kombe la Dunia ikiwa imetwaa ubingwa huo mara tano. Kadhalika, Henry ameelezea mashaka yake juu ya Ujerumani, taifa linaloshika nafasi ya pili kwa mafanikio likiwa na mataji manne ya Kombe la Dunia.
Kuhusu Ujerumani, Henry alisema bado anasubiri kuona makali yao ya zamani yakirejea chini ya kocha wao wa sasa.
"Kuhusu Ujerumani, nasubiri kuona wakirejea kwenye kiwango chao bora kabisa," aliongeza Henry. "Ujerumani imefanikiwa kufuzu, na hilo ndilo jambo la muhimu zaidi. Wakati mwingine unaweza kucheza vizuri zaidi ukiwa na presha ndogo. Vyovyote iwavyo, namtakia heri Julian Nagelsmann na timu yake – labda tu pale watakapocheza dhidi ya Ufaransa."
Silaha ya Siri ya Ufaransa: "Siri Ipo Benchi"
Alipoulizwa kuhusu nguvu kubwa zaidi ya timu ya taifa ya Ufaransa kwa sasa, Henry hakusita kujibu kuwa nguvu hiyo ipo kwenye upana wa kikosi chake (squad depth), hasa wachezaji wa akiba waliopo benchi.
"Siri ipo benchi," Henry alieleza. "Inasikika kama kitu rahisi, lakini upana wa kikosi ni jambo la msingi sana. Kama wachezaji wako wa akiba wana kiwango sawa na wale wanaoanza, hiyo ni faida kubwa sana, hasa kwenye mashindano marefu kama haya baada ya msimu mrefu na mgumu wa klabu."
Kauli ya Didier Deschamps Kuelekea Kombe la Dunia
Wakati Henry akiamini katika kikosi hicho, kocha mkuu wa Ufaransa, Didier Deschamps, anajiandaa kuongoza timu hiyo kwa mara ya nne kwenye fainali za Kombe la Dunia. Akizungumza na FIFA kuhusu mafanikio yake ya nyuma, Deschamps alisisitiza kuwa hana mpango wa kubweteka na mafanikio ya zamani.
"Mimi huwa nafikiria leo na kesho tu; ndivyo nilivyo," Deschamps alifunguka. "Kusema ukweli, mambo mengine hayajalishi. Nimejikita zaidi kwenye kile kilicho mbele yetu."
Deschamps aliongeza kuwa kumbukumbu za ubingwa wa mwaka 1998 (akiwa mchezaji) na 2018 (akiwa kocha) zitabaki moyoni mwake daima, lakini haziwezi kubadilisha ukweli kwamba soka la sasa linahitaji matokeo mapya.
"Yaliyotokea mwaka 1998 na 2018 yatabaki nami daima, lakini hakuna kinachoweza kubadilisha yaliyopita. Cha muhimu sasa ni kile tutakachofanya hapa mbele," aliongeza. "Nafasi yangu ilibadilika kati ya 1998 na 2018, lakini nilikuwepo nyakati zote mbili. Pote kulikuwa na uzoefu wa kichawi kweli kweli."
"Nimebahatika kushinda mataji katika ngazi ya klabu, ikiwemo Ligi ya Mabingwa Ulaya (Champions League) na mengineyo, lakini hakuna kitu kinachozidi kuwa bingwa wa dunia. Jina lako linabaki lile lile, lakini maneno mawili yanaongezwa milele: bingwa wa dunia."