Mambo yamezidi kuwa moto nje ya uwanja kwenye fainali za Kombe la Dunia baada ya Serikali ya Ghana kulalamikia vikali uamuzi wa Canada kumnyima visa kiungo wao tegemeo, Thomas Partey. Canada imechukua hatua hiyo kuelekea mchezo wa Black Stars dhidi ya Panama utakaopigwa wiki ijayo.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Ghana imetoa taarifa rasmi ikieleza kuwa inaelewa uamuzi huo wa Canada umechochewa na kesi ya jinai inayomkabili mchezaji huyo nchini Uingereza.
Partey, mwenye umri wa miaka 32, ambaye aliwahi kukipiga Arsenal na sasa anacheza nchini Hispania katika klabu ya Villarreal, anakabiliwa na tuhuma za ubakaji na unyanyasaji wa kijinsia nchini Uingereza, tuhuma ambazo mchezaji huyo amekuwa akizikana vikali.
Kwa sasa, Partey yuko pamoja na kikosi chake cha Ghana jijini Boston, Marekani, na atakuwa fiti kucheza mechi zinazofuata za Kundi L dhidi ya England mjini humo, pamoja na mchezo dhidi ya Croatia utakaopigwa huko Philadelphia.
Uamuzi wa Kimabavu na Usio na Haki
Wizara ya Mambo ya Nje ya Ghana imeeleza kuwa ilituma barua rasmi ya malalamiko siku ya Alhamisi ikiitaka Canada kupitia upya uamuzi huo, huku ikipanga kufungua shauri la kisheria katika Mahakama ya Shirikisho ya Canada.
Kupitia taarifa yao kwa vyombo vya habari, Serikali ya Ghana ilifunguka:
"Serikali ya Jamhuri ya Ghana inaeleza kusikitishwa kwake na uamuzi huo wa kimabavu na usio na haki hata kidogo uliochukuliwa na Canada. Huku tukiheshimu mamlaka kamili ya Canada ya kusimamia sheria zake za uhamiaji, Ghana inaona kuwa hatua ya kutegemea tuhuma ambazo hazijathibitishwa mahakamani, bila kuwepo kwa uamuzi wa kisheria, inaleta maswali mazito ya msingi kuhusu usawa na haki."
Msimamo wa Canada na FIFA
Msemaji wa Idara ya Uhamiaji, Wakimbizi na Uraia ya Canada alijibu mapigo siku ya Ijumaa kwa kusisitiza kuwa msimamo wa nchi hiyo haujabadilika, na kwamba kuwa mwenyeji wa mashindano makubwa hakubadilishi sheria zao za uhamiaji.
"Kila mtu anayeomba kuingia Canada anafanyiwa tathmini binafsi, kulingana na ukweli uliopo na sheria husika zinazofanya kazi,"- alisema msemaji huyo.
Kwa upande mwingine, Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) limejitenga na sakata hilo likisema kuwa halihusiki na taratibu za uhamiaji za nchi zinazoandaa mashindano hayo.
Changamoto za Visa Kwenye Kombe la Dunia
Sakata la Partey limekuwa tukio la hivi karibuni kabisa la mivutano ya masuala ya visa kwenye mashindano haya ya Kombe la Dunia, yanayoandaliwa kwa pamoja na nchi tatu: Canada, Marekani, na Mexico.
Hivi karibuni, Marekani ilimnyima kibali cha kuingia nchini humo mwamuzi kutoka Somalia, Omar Abdulkadir Artan, aliyekuwa amepangiwa kuchezesha mashindano hayo. Afisa mmoja kutoka serikali ya Rais Donald Trump alisema mamlaka za Marekani zilibaini kuwa mwamuzi huyo ana uhusiano na watu wanaoshukiwa kuwa wanachama wa vikundi vya kigaidi.
Baada ya kurejea Somalia, Artan alizungumzia uamuzi huo akitaja kuwa ni "kadari ya Mungu" na akawataka Wasomali wenzake wasivunjike moyo kutokana na tukio hilo.