Baada ya kukabidhiwa rasmi mikoba ya kuinoa Chelsea kwa ajili ya msimu ujao, kocha mpya Xabi Alonso amepewa ushauri wa kwanza mkubwa wa usajili ili kuirudisha klabu hiyo kwenye chati za juu za soka la Uingereza na Ulaya.
Gwiji huyo wa zamani wa Liverpool na Bayern Munich anakabiliwa na kibarua kizito cha kusuka upya kikosi cha miamba hiyo ya London Magharibi (The Blues). Chelsea inatarajiwa kulazimika kuuza baadhi ya nyota wake ili kusawazisha mahesabu ya kifedha baada ya kukosa nafasi ya kushiriki michuano ya Ulaya, lakini bado watakuwa hai sokoni kusajili majina mapya yatakayompa Alonso nafasi kubwa ya kupata mafanikio pale Stamford Bridge.
Wakati klabu hiyo ikitakiwa kuweka nguvu zaidi kwenye nafasi ya kipa na walinzi wa kati, kiungo wa zamani wa Chelsea, Andy Townsend, anaamini kuwa viongozi wa timu hiyo wanapaswa kufanya kila linalowezekana kumnasa kiungo mahiri wa Crystal Palace na timu ya taifa ya Uingereza, Adam Wharton, anayethaminiwa kufikia pauni milioni 80.
Wharton amekuwa akitajwa kuwa miongoni mwa viungo wawili wanaowindwa vikali na Manchester United (pamoja na Ederson), lakini Townsend anaamini kijana huyo ana sifa zote za kuwa nguzo kuu ya mustakabali wa Chelsea.
Pacha ya Dhahabu na Moises Caicedo
Townsend anaamini kuwa Wharton anaweza kutengeneza ushirikiano mzuri na wa kipekee na Moises Caicedo katika safu ya kiungo ya Chelsea, ushirikiano ambao utakuwa nguzo imara kwa miaka mingi ijayo.
"Naona muunganiko wa Moises Caicedo na Adam Wharton kama mustakabali wa baadaye wa Chelsea," Townsend aliiambia OLBG.
"Kama hiyo ndiyo njia ambayo Xabi Alonso anataka kuitumia, iwe katika mfumo wa 4-2-3-1 au 3-4-3, basi nina uhakika kabisa ushirikiano huo utafanya kazi vizuri sana."
Townsend amekwenda mbali zaidi na kumlinganisha Wharton na mmoja wa viungo bora zaidi kuwahi kutokea katika Ligi Kuu ya Uingereza, Michael Carrick.
"Nadhani Adam Wharton ni mchezaji wa daraja la juu sana. Ananikumbusha Michael Carrick, jinsi Carrick alivyokuwa akicheza pale Manchester United; mara zote alionekana kuwa na muda mwingi wa kutulia akiwa na mpira.
"Hakuwa mchezaji mwenye kasi kubwa sana, na ungeweza kudhani watu wangeweza kumkabili na kumnyang'anya mpira kwa urahisi, lakini hiyo haikutokea mara kwa mara. Nadhani Adam Wharton anafanana naye kwa hilo."
"Muda wa Kuondoka Umefika..."
Wharton amekuwa na msimu mzuri sana chini ya Crystal Palace, lakini Townsend anaamini huenda huu ukawa wakati sahihi kwa kijana huyo kupiga hatua nyingine mbele katika taaluma yake na kuondaka Selhurst Park.
"Kila ninapomshuhudia akicheza, mara zote anaonekana kuwa tayari na pasi inayofuata. Mara tu mpira unapomfikia, anakuwa tayari anajua nini cha kufanya," aliongeza Townsend.
"Kukosa nafasi katika kikosi cha timu ya taifa ya Uingereza kunaweza kumpa motisha ya kuhisi kuwa huu ni wakati muafaka wa kuondoka. Palace wamefurahia mafanikio hivi karibuni, na kutokana na hilo, ingekuwa na maana kubwa kwake kufanya uamuzi wa kuhama sasa.
"Nadhani mguu wake wa kushoto ukicheza sambamba na Caicedo unaweza kufanya kazi vizuri sana katika klabu kama Chelsea. Ni mchezaji mwenye talanta kubwa.
"Katika zama hizi za wachezaji wanaotegemea zaidi nguvu za mwili, inafurahisha kuona mchezaji anayeweza kutumia nguvu kiasi lakini pia akiwa na ufundi na umaridadi mkubwa katika mchezo wake. Adam Wharton anacho kitu hicho. Kama nilivyosema, mfano wa karibu zaidi ninaoweza kumpa ni Michael Carrick, anacheza kwa mtindo unaofanana sana. Nadhani atafaa sana pale Chelsea."
Kibarua sasa kinabaki kwa Xabi Alonso na bodi ya Chelsea kuona kama watakubaliana na ushauri huu na kuingia vitani dhidi ya Manchester United kuwania saini ya kinda huyo mwenye kipaji cha kipekee.